MZEE WARIOBA APIGILIA MSUMARI KWENYE SAKATA LA ESCROW

Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema pamoja na kutoa maazimio manane kuhusu uchotwaji wa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow, Bunge limefanya makosa ya kutozijumuisha Wizara ya Fedha na ile ya Viwanda na Biashara katika uchunguzi huo kwa kuwa nazo zinahusika.
Akizungumza katika mahojiano maalumu ofisini kwake Dar es Salaam jana, Jaji Warioba alitaja mambo manne aliyoyatilia shaka katika uamuzi huo wa Bunge, akisema yalilenga kulindana.
Mambo hayo ni msingi wa hukumu kwa watuhumiwa, wahusika wengine kutotajwa, mwingiliano wa mamlaka ya mihimili ya dola na wizara hizo kuachwa.
"Naona kama kulikuwa na namna fulani hivi ya kulindana. Uamuzi wa Bunge ulifikiwa kutokana na msukumo wa wananchi wa kutaka kujua hatima ya suala la escrow na IPTL, wahisani kusitisha msaada kwa sababu ya uchotwaji huo wa fedha pamoja na siasa, hasa zinazolenga urais mwaka 2015."
Jaji Warioba alisema katika ripoti ya CAG na PAC, wametaja ukiukwaji wa malipo ya kodi ya ongezeko la mtaji (capital gain) na ushuru wa stempu (stamp duty) na kuwa wanaohusika katika hilo ni Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na upande mwingine ni Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) ambao uko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.(P.T)
Alisema wanaotakiwa kuidhinisha ulipwaji wa kodi ni TRA, huku akihoji kitendo cha ripoti hizo mbili kuonyesha hisa zimeuzwa kwa Sh6 milioni wakati ilikuwa ni Dola 6 milioni, nyingine kuuzwa kwa Dola 300,000 za Marekani wakati ilikuwa Sh20 milioni.
"Hapa kuna ufisadi, maana hata kampuni iliyotajwa kuwa imesajiliwa Brela inaonyesha katika ripoti kuwa wahusika walioisajili hawakuweka majina yao, waliweka saini tu," alisema.
Alisema uamuzi wa Bunge uliilenga Wizara ya Nishati na Madini lakini hasara iliyotajwa kuonekana inazihusu zaidi Wizara ya Fedha na ile ya Viwanda.
"Kulikuwa na mchezo wa siasa, kwamba baadhi walindwe na wengine waachwe. Taarifa ya kamati imesema Kampuni ya PAP kwa kushirikiana na ofisa wa ngazi za chini wa TRA walidanganya. Hivi suala la kudanganya linafanywa na maofisa wa chini tu, kwani wa juu hawahusiki?"
Alisema kama ilivyokuwa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutakiwa kujiuzulu kwa maelezo kuwa alikuwa akifahamu mlolongo wa wizi huo, hata Hazina ilitakiwa kubanwa kwa sababu nayo ilikuwa ikifahamu suala hilo... "Tumeambiwa kuna uchunguzi unafanyika. Jambo hili bado halijafikia mwisho, iweje wengine waachwe wakati imeonekana wazi kuwa Serikali imepata hasara?"
Waliopata mgawo
Jaji Warioba alisema suala jingine lililokosa majibu ni kitendo cha watu wanaodaiwa kupewa fedha na James Rugemalira kutajwa majina yao sambamba na akaunti ya aliyewapa, lakini wale waliodaiwa kuchota fedha hizo katika magunia hawakutajwa.
"Taarifa inasema waliolipwa fedha kupitia Benki ya Stanbic walichukua fedha kwenye magunia na mfuko, sasa mbona hawajatajwa? Hata ukichukua fedha katika gunia lazima benki itabaki na kumbukumbu ya jina la aliyechukua. Tusubiri uchunguzi zaidi, ila naona kama ni dalili za kulindana.
Msingi wa uamuzi
"Ili Bunge lipate msingi wa kufanya uamuzi huo walisema fedha za escrow ni za umma na wananchi wanaelewa fedha hizo ni za umma. Binafsi nadhani katika hili Bunge halikutenda haki," alisema.
Alisema Akaunti ya Tegeta Escrow ilianzishwa kwa sababu ya mvutano kati ya Tanesco na IPTL ili kuweka fedha mpaka hapo mzozo huo utakapomalizika... "IPTL imeendelea kutoa huduma na umma umepata umeme kutoka katika kampuni hiyo na kulikuwa na malipo. Sasa kuja kumaliza tatizo lazima fedha za escrow ndiyo zingetumika kulipia gharama zote katika kipindi kile ambacho walikuwa hawajakubaliana.
"Kwa maana hiyo huwezi kusema fedha hizo ni za umma. Zilikuwa ni za kumlipa anayetoa huduma ambaye ni IPTL, sasa kwa kuwa hawakukubaliana juu ya gharama, waliamua fedha zibaki mpaka tutakapokubaliana.
"Kama fedha hizo zingekuwa za umma zingewekwa katika akaunti ya escrow kwa misingi ipi? Tusubiri uchunguzi zaidi ili tujue za umma zilikuwa kiasi gani na za watu binafsi zilikuwa kiasi gani."
Alisema kama kulikuwa na fedha za Serikali ni kodi ambayo haikuwekwa wazi.
"Hii ambayo wameeleza kwamba Serikali imepoteza Sh8 bilioni, ni kodi inayotokana na mauzo ya hisa, siyo gharama za uwekezaji. Ukiuza hisa lazima ulipe kodi ya ongezeko la mtaji na ushuru wa stempu. Hiyo ndiyo hasara wanayoisema na haihusiani na escrow kwa sababu hata kama escrow isingekuwa na matatizo, ilikuwa lazima walipe na ni utaratibu wa kawaida," alisema.
Chanzo:Mwananchi
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment