FAHAMU KWA NINI TUNAUA AKILI ASILIA NA KUKIMBILIA AKILI BANDIA
Na Mtemi Zombwe.
“...Zamani tulifundishwa mbinu za kudhibiti malaria kuwa ni kuua mazalia ya mbu ili mbu wasiwepo; leo watoto wetu wanapotoshwa kuwa mbinu ya kudhibiti malaria ni kutumia chandarua.
‘’Wanadhani watoto watavaa vyandarua wanapocheza kwenye mbu uwanjani, wanapocheza shuleni na sehemu mbalimbali.
Malaria inaendelea kuuwa watu na elimu inapotosha vizazi na vizazi, eti tiba ni chandarua. Hata wazungu waliotuambia tutumie chandarua, na wakatuletea pesa kibao za vyandarua, wao hawatumii vyandarua, wameua mazalia yote ya mbu sasa wako salama. Hii ni elimu gani inayoua akili za watoto wetu?...”
Ni nukuu kutoka kwa mkufunzi mstaafu wa Chuo cha Waalimu Morogoro, niliyefanya naye mahojiano kuhusu hali ya elimu Tanzania.
Kuua akili asilia ni kupotoshwa, kupandikizwa, kusadikishwa ujinga na nadharia mfu. Kuuawa na kuzikwa kiakili ni pale mila na tunu za asili zinapogeuzwa uongo, kufichwa kwenye shamba la ufahamu, ubunifu na kufichwa hazina ya utambuzi.
Jamii iliyozikwa huwa imezubaa na inaendelea kupata usingizi mzito licha ya kukosa dira ya maisha. Inaendelea kufundisha nadharia na masomo badala ya kufundisha ujuzi na maarifa. Inaendelea kutoa elimu bandia ya wasomi wenye vyeti pasipo ufahamu.
Tutaelimisha maelfu ya Watanzania kila siku, lakini hatutapata maendeleo licha ya kuwa na wingi wa wasomi na vyeti, kwa sababu elimu inayotolewa sasa inazika akili za Watanzania badala ya kuendelea vipaji walivyozaliwa navyo.
Nimeandika mara nyingi kuwa kuna haja ya kutafakari na kujiuliza kwanini wanafalsafa halisi na wanasayansi wa mwanzo kabisa kama vile Plato na Newton hawakusoma masomo mengi wala kuwa na digrii lukuki?
Jiulize; kwanini babu zetu ambao hawakuingia darasani kabisa lakini waliweza kuvumbua teknolojia, ufundi, kilimo, maji, uchongaji, ususi na hata kutengeneza vito vya dhahabu?
Waliweza kuzalisha chakula cha kutosheleza mahitaji yao na ya ziada, wakati hawana hata cheti cha elimu ya kilimo. Leo hii profesa wa kilimo hawezi kuzalisha hata chakula cha familia yake, ananunua chakula supamaketi!
Duniani kote, mila, utamaduni na asili za watu ndivyo vinavyowaongoza kupata michepuo ya akili zao (intellectual faculties)na siyo michepuo ya masomo, au elimu ya darasani. Ndiyo maana watu wote walioendelea duniani wanatunza na kutii mila asilia za utamaduni waliozaliwa nao na kukulia.
Mifano iko hai; Wazungu na wahindi walioko Afrika bado wanatii mifumo asili ya akili, mila na utamaduni wao popote walipo na wakati wote. Hata watoto wadogo wanaozaliwa wanaijua na kuitafsiri dunia kwa kutumia mifumo asili, mila na tamaduni zilizowazunguka. Ndizo zinakuza akili, ufahamu, utambuzi na vipaji.
Eti miradi ya kilimo inaandikwa na maprofesa wa kilimo na uchumi ambao hawajawahi kulima wala hawana mashamba.
Wanakaa kwenye mahoteli makubwa na kulipwa posho kubwa. Wanaandika programu ya kilimo kwa Kiingereza ambayo haitekelezeki wala haifanani na uhalisia wa kilimo chetu. Umaskini unabaki palepale.
Kama wangechukuliwa wakulima wenyewe (wenye elimu sahihi ya kilimo) hata kama hawajui kusoma na kuandika wangetoa mpango wa kuboresha kilimo ambao ni sahihi, unaotekelezeka na wenye manufaa makubwa kwa wakulima. Elimu ya maandishi inadidimiza Afrika!
Hatuwezi kukwepa kujadili na kufundisha watoto wetu ukweli kuhusu vyanzo vya utambuzi, ufahamu, uelewa na ubunifu duniani. Lazima tujue na watoto wetu wajue mizizi ya utambuzi iko wapi?
0 comments:
Post a Comment