Hata kama umbile lako lilikuwa kubwa kiasi gani kabla na baada ya ujauzito, huna budi kusubiri kwa kipindi hicho.
Wanawake wengi wanaojifungua kwa upasuaji, hukumbana na changamoto kubwa ya kurudisha miili yao katika hali ya kawaida. Hali hii husababishwa na muda wa kuuguza kidonda na hofu ya kujitonesha.
Wataalamu wa afya kutoka Kituo cha Malezi na Ushauri cha Hispania (CMA) wanaeleza kuwa ni lazima mama aliyejifungua kwa upasuaji achukue tahadhari kubwa kabla ya kufanya mazoezi yoyote.
Awe karibu na daktari wake ili amuulize maswali kadhaa kabla ya kujichukulia uamuzi kuhusu mwili wake katika kipindi hicho.
Mama aliyejifungua kwa upasuaji anashauriwa kusubiri kwa wiki sita kabla ya kuanza mazoezi.
Hata kama umbile lako lilikuwa kubwa kiasi gani kabla na baada ya ujauzito, huna budi kusubiri kwa kipindi hicho.
Kubeba mtoto na kuzaa kunaathiri, lakini upasuaji husababisha mwili kufubaa na kuzorota. Hiyo ni changamoto inayomlazimisha mtu kujipanga ili kurudia hali yake aliyokuwa nayo awali.
Jambo la msingi ni mhusika kushauriana na daktari wake kabla ya kuanza mazoezi. Miongoni mwa mambo yatakayozingatiwa kabla ya mazoezi ni kidonda kupona ili kisitoneshwe kwa mazoezi.
Hata hivyo, kuna mazoezi mepesi ambayo mgonjwa anaweza kujipima mwenyewe kwa kuhakikisha anauweka vyema mwili wake.
Hii ni pamoja na kufanya mazoezi ya kutembea hapa na pale kama vile kando ya uwanja pembeni mwa nyumba.
Zoezi hili ni zuri tu kwa kukurudisha mtu katika hali ya kawaida na kumpa hamu ya mazoezi baada ya upasuaji lakini pia ni njia nzuri ya kupata hewa safi.
Kuna mazoezi ya sakafuni, kupiga msamba ambayo yatasaidia kuimarisha misuli inayozunguka maeneo ya uke na mapaja. Misuli hii ndiyo inayokuwezesha kudhibiti mkojo.
Mazoezi yasiyoweza kuleta maumivu kwenye viungo lakini bado yakakuweka katika umbile zuri, kwa mfano kuogelea. Unaweza kuendesha baiskeli pia au kukimbia.
Kama ilivyo kwa wanawake waliojifungua kwa upasuaji, ndivyo inavyotakiwa kuwa kwa mtu mwingine yeyote ambaye ameugua na kulazwa kwa matibabu. Mara baada ya kupata nafuu na kuweza kutembea, anapaswa kufanya mazoezi polepole ili kuurejesha mwili katika hali yake ya kawaida.
Akiwa anafanya mazoezi mepesi itakuwa rahisi kuendeleza mazoezi aliyokuwa anafanya awali bila kuwa na shida.
Hivyo ni kusema mtu yoyote anapaswa kufanya mazoezi kulingana na uwezo alio nao kwa lengo la kuuweka mwili katika hali nzuri ya kiutendaji.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment